Udukuzi wa DAO: hadithi ya Ethereum Asilia
Hadithi ya udukuzi wa DAO mwaka 2016, na jinsi mwitikio wa jamii ulivyosababisha kuundwa kwa Ethereum Asilia kama mnyororo tofauti.
Date published: 15 Desemba 2021
Maelezo kutoka kwa Junion yanayosimulia hadithi ya udukuzi wa DAO mwaka 2016, moja ya wizi mkubwa zaidi wa kidijitali katika historia ya kripto, na jinsi uamuzi wenye utata wa jamii ya Ethereum wa kuchepusha mnyororo wa vitalu ulivyosababisha kuundwa kwa Ethereum Asilia.
Nakala hii ni nakala inayofikika ya nakala asili ya video (opens in a new tab) iliyochapishwa na Junion. Imehaririwa kidogo ili isomeke vizuri.
Ugunduzi (0:00)
Ni Jumatatu, Juni 13, 2016. Profesa wa sayansi ya kompyuta katika chuo cha Cornell anachunguza msimbo wa DAO, moja ya miradi yenye malengo makubwa zaidi katika nafasi ya kripto. Kwa miezi kadhaa alikuwa akitetea mradi huo usitishwe, kwani aliamini kulikuwa na kasoro fulani ambazo zingeweza kuweka mradi mzima hatarini. Lakini leo anapata udhaifu mkubwa: hitilafu kwenye mstari wa 666.
Anahofia kwamba hitilafu hii inaweza kumruhusu mdukuzi kufanya utoaji wa pesa usio na kikomo kama kwenye ATM. Hata kama mshambuliaji alikuwa na dola 10 tu kwenye akaunti yake, angeweza kuitoa tena na tena na tena hadi pesa zote ziishe. Kulikuwa na robo bilioni ya dola iliyowekezwa kwenye DAO, na kila senti ilikuwa hatarini.
Slock.it, kampuni iliyo nyuma ya DAO, inakubali uwezekano wa unyonyaji huo lakini inatangaza kwamba shambulio lolote halingewezekana, hivyo fedha zote bado ziko salama. Wanafanya mabadiliko kwenye GitHub kwa kubadilishana mistari miwili ya msimbo — suluhisho ambalo litajumuishwa kama sehemu ya Mfumo wa DAO toleo la 1.1.
Lakini wakati timu ikidai ushindi, mdukuzi alikuwa akifuata nyayo zao kwa siri, akitengeneza unyonyaji unaotumia fursa ya hitilafu hii hii. Sasa ni Ijumaa, siku nne baadaye, na DAO imedukuliwa kwa kiasi cha dola milioni 55.
Kama vile udukuzi wa SWIFT wa dola milioni 81 ulivyotangaza mapengo katika sekta ya benki iliyowekwa kati, na shambulio la programu ya ukombozi la WannaCry lilivyofichua udhaifu mkubwa katika mifumo ya uendeshaji ya kompyuta, udukuzi wa DAO ulifichua udhaifu wa mapema wa usalama wa mkataba mahiri katika ulimwengu ambapo msimbo unaamuru kila kitu. Iliiacha jamii ya Ethereum ikiwa imevunjika moyo huku wakihaha kujaribu kurejesha udhibiti wa mnyororo wa vitalu.
Hii ni hadithi ya moja ya wizi mkubwa zaidi wa kidijitali kuwahi kutokea na jaribio la ujasiri la kuandika upya historia ili isionekane kama ilitokea.
DAO ilikuwa nini? (2:00)
Ingia kwenye DAO — kifupi cha shirika linalojitegemea lililogatuliwa. Wazo hili lilitokana na uchangiaji wa umma. Badala ya fedha nyingi kwa miradi tofauti, kungekuwa na mfuko mmoja wa kuzitawala zote, na hakukuwa na njia bora ya kufanya hivi zaidi ya kutumia DAO.
Wakati wa uzinduzi, wawekezaji wangepokea tokeni 100 za DAO kwa kila Etha iliyowekwa. Tokeni hizi ziliwapa utawala juu ya itifaki na ziliwakilisha hisa zao za DAO. Wamiliki wa tokeni wangeweza kuwasilisha mapendekezo — kwa mfano, ungeweza kutoa pendekezo la kuwekeza dola milioni moja badala ya asilimia 10 ya dhamana katika kampuni XYZ.
Mara tu pendekezo lilipopita uthibitisho wa awali, lingepigiwa kura na wawekezaji wengine wote. Katika kipindi hiki, wamiliki wa tokeni wangeweza kupiga kura ya ndiyo ikiwa waliamini uwekezaji huo ulileta thamani chanya iliyotarajiwa, au hapana ikiwa waliamini ulileta thamani hasi iliyotarajiwa. Wangeweza pia kutumia jukwaa kutoa maoni yao na kusoma ya wengine.
Wakati kipindi cha kupiga kura kilipoisha na akidi ya 20% ya tokeni zote ilipofikiwa, DAO ilihamisha Etha iliyobainishwa kiotomatiki kwenda kwenye mkataba mahiri uliowakilisha pendekezo hilo. Etha yoyote iliyotokana na mapendekezo haya ingerudishwa kwenye hazina. Ilikuwa kama mfuko mmoja mkubwa wa uwekezaji uliogatuliwa, ulioundwa kupata faida. Wazo lilikuwa kwamba hekima ya umati ingesaidia kuunda fursa bora za uwekezaji.
Hata hivyo, bado kulihitajika njia ya kuwalinda walio wachache dhidi ya kukandamizwa na walio wengi. Ikiwa kikundi cha wachache hakikubaliani kabisa na pendekezo ambalo hawangeweza kulishinda kwa kura, badala ya kupiga kura ya hapana, wangeweza kuita utendakazi wa kugawanya na kuhamisha Etha yao kutoka kwenye DAO kuu kwenda kwenye DAO tanzu, kimsingi wakiigawanya DAO mara mbili. Utendakazi huu wa kugawanya utakuwa muhimu sana baadaye.
Uchangiaji wa umma (4:01)
DAO ulikuwa mradi mkubwa zaidi wa uchangiaji wa umma kuwahi kutokea, ukikusanya Etha milioni 12.7 — yenye thamani ya dola milioni 150 kwa wakati huo. Ilifanyika wakati wa enzi za mwanzo za Ethereum, ambapo mradi huo ulikabiliwa na kiasi kikubwa cha msisimko na hofu ya kupitwa (FOMO) ya wawekezaji.
Kabla ya hili, miradi ya Ethereum ilikuwa hasa uthibitisho wa dhana tu, lakini huu ulikuwa mradi unaofanya kazi kikamilifu wenye uwezo mkubwa. Ulikuwa salama kabisa dhidi ya udukuzi wowote, ukilindwa na mamilioni ya wachimbaji kote ulimwenguni, na ulikuwa umeogatuliwa — mradi mzima uliundwa na mfululizo wa mikataba mahiri kwenye Ethereum.
Huu ulikuwa msimbo usiobadilika uliopangishwa kwenye kompyuta salama zaidi ulimwenguni, ambao ulihakikisha sifa kuu za DAO: shirika ambalo limegatuliwa kabisa na linajitegemea. Mara tu mikataba ilipotumwa mnamo Aprili 30, hakuna chombo kimoja — hata Slock.it — kingeweza kufanya mabadiliko kwenye itifaki au kusimamisha uwepo wake. Msimbo wake ulikuwa umekaguliwa mara nyingi na watengenezaji mbalimbali wa Ethereum na uliweza kuonekana na kila mtu kwa ukaguzi.
Udukuzi (5:02)
"Pweke, pweke sana" — jina la Pendekezo la DAO #59. Ni pendekezo la kawaida tu la kugawanya, lakini kwa kweli ndipo udukuzi unapoanzia. Baada ya mdukuzi kuwasilisha pendekezo, kuna kipindi cha kawaida cha siku saba cha mjadala ambapo mtu yeyote yuko huru kujiunga. Hata hivyo, hakuna anayejiunga na mgawanyiko huu.
Ni utaratibu wa kawaida kwa mtu kuita mgawanyiko peke yake, kuunda DAO tanzu, na kisha kuunda pendekezo ambalo linatuma Etha yote kurudi kwenye mkoba wao. Hii inaruhusu mtumiaji kudai tena pesa zao zinazoungwa mkono na tokeni zao za DAO. Siku saba sasa zimepita, na mdukuzi sasa anaruhusiwa kuita utendakazi wa kugawanya. Hakuna anayeshuku chochote.
Hata hivyo, utendakazi wa kugawanya unapoitwa, jamii inagundua jambo la kutisha. Etha inavujishwa kutoka kwenye DAO kwa kasi ya dola milioni nane kwa saa. Jamii inahaha kujua nini kinaendelea. Inaonekana mshambuliaji anaita utendakazi wa kugawanya kwa kujirudia — tena na tena na tena, mamia ya mara.
Unakumbuka lile suluhisho la hitilafu lililofanyika siku nne zilizopita? Ni aibu kwamba hakuna njia ya kuhariri msimbo wa mkataba mahiri baada ya kutumwa, kwa hivyo suluhisho hili lilikuwepo tu kwenye GitHub kama sehemu ya The DAO 1.1, DAO tofauti kabisa iliyokuwa ikitengenezwa. Suluhisho hili dogo lingeweza kuzuia jambo zima — lilichofanya ni kubadilishana mistari miwili ya msimbo ili salio lisasishwe kabla ya malipo halisi.
Lakini bila suluhisho hili, mtu yeyote angeweza kuita utendakazi mara kwa mara ili kutoa Etha kabla ya mkataba kusasisha salio lao. Ni kama ATM ambayo haibadilishi salio lako hadi ikupe pesa. "Je, ninaweza kutoa dola kumi? Subiri, kabla ya hapo, ninaweza kutoa dola kumi? Subiri, kabla ya hapo…"
Kikundi cha Robin Hood (6:55)
Wamiliki wa tokeni za DAO walitazama huku uwekezaji wao ukivujishwa polepole kutoka kwenye DAO kuu kwenda kwenye DAO tanzu, inayojulikana pia kama DAO nyeusi. Zaidi ya hayo, bei ya Ethereum ilishuka ghafla kutoka dola 20 hadi dola 15 kufuatia habari hizo. Kitu kilihitajika kufanywa, na njia pekee ilikuwa ni kuvujisha kilichosalia kabla mdukuzi hajafanya hivyo. Na hivyo ndivyo mbio za kukausha zilianza.
Upande mwingine wa dunia, katika nyumba yake katika kitongoji cha Copacabana huko Rio de Janeiro, Alex Van de Sande anaamka na kukuta simu yake imejaa jumbe za Skype. Anamgeukia mke wake na kusema, "Unakumbuka nilipokuwa nikikuambia kuhusu lile rundo kubwa la pesa lisiloweza kudukuliwa? Limedukuliwa."
Alex aliwasiliana na watengenezaji wengine ambao hawakutajwa majina na wakaunda kikundi walichokipa jina la utani la Robin Hood — wadukuzi wema ambao wangevujisha fedha zilizosalia na kuzirudisha kwa wamiliki halali. Hata hivyo, hawakuwa na muda wa kupendekeza mgawanyiko mpya, kwani hilo lingehitaji kipindi cha siku saba cha kupiga kura.
Badala yake, walielekeza macho yao kwenye Pendekezo #71, ambalo lilikuwa karibu kuisha ndani ya saa chache. Wangejiunga na mgawanyiko huo na kutumia udukuzi huo huo kufyonza fedha zote zilizosalia kwenye DAO hii tanzu. Saa sita zilikuwa zimepita tangu shambulio lianze, na mwizi alikuwa amefanikiwa kuiba 30% ya Etha ya DAO. Lakini kwa sababu isiyojulikana, shambulio liliacha kufanya kazi. Miamala ilishindwa na yote yakafikia kikomo.
Wakati huo huo, Alex alikuwa akijiandaa kuanzisha shambulio la wadukuzi wema ili kulinda 70% ya fedha zilizosalia. Lakini ghafla alipoteza muunganisho wake wa intaneti. Akiwa amebakiza dakika 30 tu, alipiga simu kwa wasiwasi kwa NET, mtoa huduma wake wa intaneti wa Brazili, lakini alipata tu jibu kutoka kwa sauti ya roboti: "Tunaona kuna tatizo la intaneti katika mtaa wako." Pendekezo la kugawanya liliisha na alikuwa amekosa fursa ya kutekeleza shambulio la Robin Hood.
Asubuhi iliyofuata, Alex alijaribu kukusanya tena kikundi ili kupenyeza kwenye pendekezo lingine la kugawanya, lakini wengine walikuwa na shughuli nyingi. "Tulijihisi kama wadukuzi wabaya zaidi katika historia. Tulikwamishwa na intaneti mbaya na majukumu ya kifamilia."
Mbio za kumaliza (9:10)
Siku nne baada ya shambulio la awali, DAO ilishambuliwa tena. Ilikuwa ikivuja polepole — Etha chache kwa kila mzunguko — lakini ilikuwa tayari imekusanya maelfu ya dola. Ilionekana kuwa kutoka kwa mshambuliaji anayejaribu mazingira. Katika hatua hii, Robin Hood alihitaji kufanya kitu.
Walichagua kupenyeza kwenye Mgawanyiko #78 kwa sababu walikuwa wamemtambua msimamizi wa pendekezo na lilikuwa linaisha hivi karibuni. Waliwasiliana na baadhi ya wawekezaji wakubwa ambao walifurahi kuchangia tokeni zao za DAO, na kuruhusu timu kupata tokeni milioni sita. Kadiri mkataba wa Robin ulivyokuwa na tokeni nyingi, ndivyo ulivyoweza kufyonza Etha kwa haraka zaidi. Mshambuliaji aliongeza kasi na washambuliaji wengine walijiunga. Lakini kutokana na michango hiyo, Robin Hood aliweza kuwapita. Hii iliwaruhusu kulinda Etha milioni 7.2 — 55% ya DAO.
Mchepuo (10:08)
DAO kuu sasa ilikuwa imevujishwa na fedha zote zilisambazwa kwenye DAO tanzu kadhaa — mbili kuu zikiwa DAO ya wadukuzi wema na DAO nyeusi. Lakini pesa zote zilikuwa zimefungwa kwa muda. Hakuna pendekezo ambalo lingeweza kuwasilishwa chini ya DAO tanzu hadi kipindi cha kusubiri cha siku 27 kiishe. Na hata baada ya hapo, kutuma fedha kwenye anwani ya nje kulihitaji kuwasilisha pendekezo na kusubiri kwa wiki mbili. Kimsingi, bado kulikuwa na siku 41 hadi mdukuzi aweze kutoa pesa ambazo zililingana na 5% ya usambazaji wote wa Ethereum.
Lakini mdukuzi hangekuja kugusa Ethereum yake. Kilichotokea baadaye ni moja ya matukio ya ujasiri na yenye utata zaidi katika historia ya mnyororo wa vitalu. Jamii iliamua kwamba hawangemruhusu mdukuzi ashinde. Walitaka kuandika upya historia ili kila muamala uliohusika katika udukuzi huo ubatilishwe, na kila mtu apate pesa zake. Walichagua kuchepusha Ethereum.
Mnyororo wa vitalu ni kama orodha ya miamala inayoendelea kukua kwa kila kitalu kinachochimbwa. Kila muamala umekita mizizi katika mnyororo wa vitalu milele. Lakini ikiwa zaidi ya 50% ya wachimbaji watashirikiana, wanaweza kubadilisha mnyororo wa vitalu kwa udanganyifu, wakiandika upya historia jinsi wanavyotaka. Kawaida hii inaitwa shambulio la asilimia 51. Lakini hakukuwa na nia mbaya kuhusu mchepuo huu — jamii ilikuwa inarudisha tu pesa zilizoibiwa kutoka kwao.
Msimbo ni sheria (11:48)
Bado, si kila mtu alikubaliana na mchepuo uliopendekezwa. Walidai kwamba msimbo ni sheria. Katika mtazamo huu, mshambuliaji hakuwa mdukuzi sana bali alikuwa kama mwanasheria mwerevu aliyesoma kwa makini masharti ya mkataba. Kwa hivyo, hakuna fedha zilizokuwa zimeibiwa kweli na walipaswa kuwa na haki halali ya Etha kutoka kwenye DAO nyeusi.
Ni muhimu kutambua kwamba Ethereum yenyewe haikuwahi kudukuliwa — ulikuwa tu mkataba mahiri ulioandikwa vibaya ambao ulitumiwa vibaya. Vitu viwili tofauti. Zaidi ya hayo, waliamini kwamba mambo yanayotokea kwenye mnyororo wa vitalu hayabadiliki na hayapaswi kuchezewa bila kujali hali.
Siku moja baada ya shambulio la awali, mshambuliaji alituma barua ya wazi katika soga ya kikundi cha Slack cha DAO, iliyotiwa saini na ufunguo wa siri wao:
"Kwa DAO na jamii ya Ethereum: Nimechunguza kwa makini msimbo wa The DAO na nimedai kwa haki Etha milioni 3, na ningependa kuishukuru DAO kwa tuzo hii. Nimesikitishwa na wale wanaoelezea matumizi ya kipengele hiki cha makusudi kama 'wizi.' Ninatumia kipengele hiki kilichowekwa wazi kwenye msimbo kulingana na masharti ya mkataba mahiri. Mchepuo laini au mchepuo mgumu utakuwa sawa na kunyang'anywa Etha yangu halali na ya haki. Mchepuo kama huo utaharibu kabisa na bila kurekebishika imani yote si tu kwa Ethereum bali pia katika uwanja wa mikataba mahiri na teknolojia ya mnyororo wa vitalu. Usifanye kosa: mchepuo wowote, laini au mgumu, utaharibu zaidi Ethereum na kuharibu sifa na mvuto wake."
Baada ya ukaguzi zaidi, watu waligundua kuwa sahihi ilikuwa batili, kwa hivyo barua hii iliandikwa tu na mtu anayedai kuwa mshambuliaji.
Kwa upande mwingine, watetezi walidai kwamba "msimbo ni sheria" ni kauli kali sana na kwamba binadamu wanapaswa kuwa na kauli ya mwisho kupitia mwafaka wa kijamii. Mdukuzi hapaswi kuruhusiwa kufaidika na unyonyaji huo kwani ni makosa kimaadili na kuna uwezekano mkubwa ni kinyume cha sheria. Lakini muhimu zaidi, DAO ilikuwa kubwa mno kushindwa. Ilishikilia karibu 15% ya usambazaji wote wa Etha.
Ethereum Asilia (14:34)
Katika tukio ambalo liliakisi mgogoro wa kifedha wa 2008, watengenezaji wa Ethereum waliokoa DAO. Vitalik Buterin, muundaji na mtengenezaji mkuu wa Ethereum, hakuomba radhi kuhusu kushinikiza mchepuo. Katika mahojiano, baadaye alisema, "Baadhi ya watumiaji wa Bitcoin wanaona mchepuo mgumu kama kwa njia fulani unakiuka maadili yao ya msingi. Binafsi nadhani maadili haya ya msingi, yakisukumwa kwa viwango hivyo, ni ya kijinga."
Maoni haya yalitawala wengi katika jamii ya Ethereum. Kura yenye utata ya jamii — ambapo Etha moja ni sawa na kura moja — ilionyesha 87% ya kuunga mkono mchepuo. Kwa hivyo kwenye kitalu 1,920,000, nodi za kompyuta kote ulimwenguni zilisasisha programu zao na kukubali mchepuo. Etha yote kutoka kwenye DAO na DAO tanzu ilihamishiwa kwenye mkataba wa kurejesha fedha.
Lakini haiishii hapo. Mnyororo wa vitalu asili wa Ethereum — ule wenye udukuzi wa DAO — uliendelea. Kwa kweli, ulikuwa unakua. Wachimbaji waliopinga mchepuo waliendelea kuchimba vitalu na miamala ilikuwa bado inafanywa. Siku iliyofuata, Poloniex iliorodhesha sarafu hiyo na ikaanza kufanyiwa biashara kwa dola 2 kila moja. Mnyororo huu ulijulikana kama Ethereum Asilia — mnyororo wa vitalu asili, usiobadilishwa.
Ikiwa ulishikilia Etha kabla ya mchepuo, sasa ungekuwa na Ethereum moja na Ethereum Asilia moja. Ikiwa ulishikilia Etha moja kwenye DAO, ungeweza kutoa Ethereum moja kutoka kwenye mkataba wa kurejesha fedha. Na ikiwa ulikuwa umedukua DAO, ungekuwa umetengeneza utajiri mzuri katika Ethereum Asilia — karibu dola milioni saba.
Urithi wa DAO (16:14)
Hapo awali, Ethereum Asilia ilipata kasi kama mbadala, ikiwa na jamii yenye nguvu ya wenye msimamo mkali wa mnyororo wa vitalu ambao hawakukubaliana na uokoaji. Lakini tangu wakati huo, Ethereum Asilia imeshindwa kupata mvuto na inakuwepo tu kama wazo lenye matumizi madogo. Wakati Ethereum ni nyumbani kwa maelfu ya itifaki, Ethereum Asilia ina chache tu za msingi. Ni wazi kwamba mchepuo ulikuwa umeshinda.
Miezi miwili baadaye, Robin Hood walihamisha milioni 2.9 za Ethereum Asilia yao kwenda Poloniex na kuiuza yote kwa Ethereum katika jaribio la kushusha bei. 14% ilibadilishwa kwa mafanikio, lakini 86% ilizuiliwa na Poloniex na kurudishwa kwa kikundi. Robin Hood walianzisha mkataba wa kurejesha fedha kwenye mtandao wa Ethereum Asilia kwa watumiaji walioathiriwa na udukuzi wa DAO.
Kuhusu mdukuzi, aliondoka na Ethereum Asilia milioni 3.6 — yenye thamani ya dola milioni 150 leo. Lakini kama kusingekuwa na mchepuo, Ethereum hiyo milioni 3.6 ingekuwa na thamani ya zaidi ya dola bilioni saba leo.
Athari ya kudumu ya DAO (17:26)
Ni muhimu kutambua kwamba DAO sasa inajulikana kama Genesis DAO ili kuepuka mkanganyiko, kwa sababu ilikuwa DAO ya kwanza lakini hakika si ya mwisho. Licha ya vikwazo vya awali, DAO zimezidi kuwa maarufu. MakerDAO inatawala sarafu thabiti ya DAI, na itifaki za fedha zilizogatuliwa (DeFi) kama vile Uniswap yenye tokeni yake ya UNI kwa kawaida huwa na DAO ya utawala. DAO hizi zote zilijengwa kutokana na uzoefu wa miradi ya awali ili kuunda mashirika yenye matumizi mengi na yenye mafanikio zaidi.
Lakini Genesis DAO ilikuwa ya kwanza ya aina yake, iliyoundwa kama jaribio — la gharama kubwa — ikidhibiti dola milioni 250 katika kilele chake, au 15% ya usambazaji wote wa Ethereum. Christoph Jentzsch, mtengenezaji mkuu, alitarajia tu ikusanye dola milioni tano na baadaye alisema anajutia kutoiwekea kikomo. Kwa jaribio kubwa kama hilo, ilikuwa mapema mno na hakika ilikuwa kubwa mno kushindwa.
Kuunda mkataba mahiri ni kama kutengeneza gari linalojiendesha — ni jukumu kubwa linalohitaji majaribio ya kina ili kuepuka ajali. Hata kwa tahadhari hii mpya, itifaki za fedha zilizogatuliwa (DeFi) bado zinadukuliwa kwa zaidi ya dola milioni 50, baadhi hata baada ya kukaguliwa na makampuni ya kitaalamu ya ukaguzi. Lakini tangu udukuzi wa DAO, hakujawa na uokoaji mwingine. Jamii ya Ethereum ina nguvu zaidi sasa na iko tayari kuendelea na miradi mikubwa zaidi na yenye malengo makubwa, ikijenga kizazi kijacho cha programu za kidijitali.