Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Jinsi Unganisho lilivyoathiri usambazaji wa ETH

Unganisho liliwakilisha mpito wa mtandao wa Ethereum kutoka Uthibitisho wa Kazi (PoW) kwenda Uthibitisho wa Dau (PoS) uliotokea Septemba 2022. Njia ambayo ETH ilitolewa ilipitia mabadiliko wakati wa mpito huo. Hapo awali, ETH mpya ilitolewa kutoka vyanzo viwili: tabaka la utekelezaji (yaani, Mtandao Mkuu) na tabaka la mwafaka (yaani, Mnyororo wa Beacon). Tangu Unganisho, utoaji kwenye tabaka la utekelezaji sasa ni sifuri. Hebu tuchanganue hili.

Vipengele vya utoaji wa ETH

Tunaweza kugawanya usambazaji wa ETH katika nguvu mbili kuu: utoaji na kuteketeza.

Utoaji wa ETH ni mchakato wa kuunda ETH ambayo haikuwepo hapo awali. Kuteketeza ETH ni wakati ETH iliyopo inaharibiwa, na kuiondoa kwenye mzunguko. Kiwango cha utoaji na kuteketeza kinahesabiwa kwa vigezo kadhaa, na usawa kati yao huamua kiwango kinachotokana cha mfumuko wa bei/kushuka kwa bei ya Etha.

ETH issuance tldr

  • Kabla ya kuhamia kwenye Uthibitisho wa Dau (PoS), wachimbaji walitolewa takriban ETH 13,000 kwa siku
  • Waweka dhamana wanatolewa takriban ETH 1,700 kwa siku, kulingana na takriban jumla ya ETH milioni 14 zilizowekwa dhamana
  • Utoaji halisi wa uwekaji dhamana hubadilika kulingana na jumla ya kiasi cha ETH kilichowekwa dhamana
  • Tangu Unganisho, ni takriban ETH 1,700 tu kwa siku inayosalia, na kushusha jumla ya utoaji mpya wa ETH kwa takriban 88%
  • Kuteketeza: Huku hubadilika kulingana na mahitaji ya mtandao. Ikiwa wastani wa bei ya gesi ya angalau Gwei 16 inazingatiwa kwa siku fulani, hii inafidia kikamilifu takriban ETH 1,700 inayotolewa kwa wathibitishaji na kuleta mfumuko halisi wa ETH kuwa sifuri au chini ya hapo kwa siku hiyo.

Kabla ya unganisho (kihistoria)

Utoaji wa tabaka la utekelezaji

Chini ya Uthibitisho wa Kazi (PoW), wachimbaji waliingiliana tu na tabaka la utekelezaji na walipewa tuzo za kitalu ikiwa walikuwa wachimbaji wa kwanza kutatua kitalu kinachofuata. Tangu sasisho la Konstantinopoli mnamo 2019 tuzo hii ilikuwa ETH 2 kwa kila kitalu. Wachimbaji pia walipewa tuzo kwa kuchapisha vitalu vya , ambavyo vilikuwa vitalu halali ambavyo havikuishia kwenye mnyororo mrefu zaidi/mnyororo mkuu. Tuzo hizi zilifikia ukomo wa ETH 1.75 kwa kila ommer, na zilikuwa pamoja na tuzo iliyotolewa kutoka kwa kitalu kikuu. Mchakato wa uchimbaji ulikuwa shughuli kubwa kiuchumi, ambayo kihistoria ilihitaji viwango vya juu vya utoaji wa ETH ili kudumisha.

Utoaji wa tabaka la mwafaka

Mnyororo wa Beacon ulianza kufanya kazi mnamo 2020. Badala ya wachimbaji, unalindwa na wathibitishaji wanaotumia Uthibitisho wa Dau (PoS). Mnyororo huu ulianzishwa na watumiaji wa Ethereum wakiweka ETH kwa njia moja kwenye mkataba mahiri kwenye Mtandao Mkuu (tabaka la utekelezaji), ambao Mnyororo wa Beacon unasikiliza, na kumpa mtumiaji kiasi sawa cha ETH kwenye mnyororo mpya. Hadi Unganisho lilipotokea, wathibitishaji wa Mnyororo wa Beacon hawakuwa wakichakata miamala na kimsingi walikuwa wakifikia mwafaka juu ya hali ya kundi la wathibitishaji lenyewe.

Wathibitishaji kwenye Mnyororo wa Beacon wanapewa tuzo ya ETH kwa kuthibitisha hali ya mnyororo na kupendekeza vitalu. Tuzo (au adhabu) huhesabiwa na kusambazwa katika kila kipindi (kila dakika 6.4) kulingana na utendaji wa mthibitishaji. Tuzo za mthibitishaji ni ndogo sana kuliko tuzo za uchimbaji ambazo zilitolewa hapo awali chini ya Uthibitisho wa Kazi (PoW) (ETH 2 kila takriban sekunde 13.5), kwani kuendesha nodi ya kuthibitisha sio kubwa kiuchumi na hivyo haihitaji au kustahili tuzo kubwa kiasi hicho.

Mchanganuo wa utoaji kabla ya unganisho

Jumla ya usambazaji wa ETH: ~ETH 120,520,000 (wakati wa Unganisho mnamo Septemba 2022)

Utoaji wa tabaka la utekelezaji:

  • Ilikadiriwa kuwa ETH 2.08 kwa kila sekunde 13.3*: ~ETH 4,930,000 zilitolewa kwa mwaka
  • Ilisababisha kiwango cha mfumuko wa bei cha takriban 4.09% (Milioni 4.93 kwa mwaka / jumla ya Milioni 120.5)
  • *Hii inajumuisha ETH 2 kwa kila kitalu kikuu, pamoja na wastani wa ETH 0.08 kwa muda kutoka kwa vitalu vya ommer. Pia inatumia sekunde 13.3, lengo la msingi la muda wa kitalu bila ushawishi wowote kutoka kwa . (Tazama chanzo (opens in a new tab))

Utoaji wa tabaka la mwafaka:

  • Kwa kutumia jumla ya ETH 14,000,000 zilizowekwa dhamana, kiwango cha utoaji wa ETH ni takriban ETH 1700 kwa siku (Tazama chanzo (opens in a new tab))
  • Inasababisha ~ETH 620,500 kutolewa kwa mwaka
  • Ilisababisha kiwango cha mfumuko wa bei cha takriban 0.52% (620.5K kwa mwaka / jumla ya Milioni 119.3)

Jumla ya kiwango cha utoaji kwa mwaka (kabla ya unganisho): ~4.61% (4.09% + 0.52%)

~88.7% ya utoaji ilikuwa ikienda kwa wachimbaji kwenye tabaka la utekelezaji (4.09 / 4.61 * 100)

~11.3% ilikuwa ikitolewa kwa waweka dhamana kwenye tabaka la mwafaka (0.52 / 4.61 * 100)

Baada ya unganisho (siku hizi)

Utoaji wa tabaka la utekelezaji

Utoaji wa tabaka la utekelezaji tangu Unganisho ni sifuri. Uthibitisho wa Kazi (PoW) sio tena njia halali ya uzalishaji wa kitalu chini ya sheria zilizoboreshwa za mwafaka. Shughuli zote za tabaka la utekelezaji zimefungwa katika "vitalu vya beacon", ambavyo vinachapishwa na kuthibitishwa na wathibitishaji wa Uthibitisho wa Dau (PoS). Tuzo za kuthibitisha na kuchapisha vitalu vya beacon zinahesabiwa kando kwenye tabaka la mwafaka.

Utoaji wa tabaka la mwafaka

Utoaji wa tabaka la mwafaka unaendelea leo kama kabla ya Unganisho, na tuzo ndogo kwa wathibitishaji wanaothibitisha na kupendekeza vitalu. Tuzo za mthibitishaji zinaendelea kujilimbikiza kwenye salio la mthibitishaji ambalo linasimamiwa ndani ya tabaka la mwafaka. Tofauti na akaunti za sasa (akaunti za "utekelezaji"), ambazo zinaweza kufanya miamala kwenye Mtandao Mkuu, hizi ni akaunti tofauti za Ethereum ambazo haziwezi kufanya miamala kwa uhuru na akaunti zingine za Ethereum. Fedha katika akaunti hizi zinaweza tu kutolewa kwa anwani moja maalum ya utekelezaji.

Tangu sasisho la Shanghai/Capella lililofanyika Aprili 2023, utoaji huu umewezeshwa kwa waweka dhamana. Waweka dhamana wanahamasishwa kuondoa mapato/tuzo zao (salio la zaidi ya ETH 32) kwani fedha hizi vinginevyo hazichangii kwenye uzito wao wa dhamana (ambao unafikia ukomo wa 32).

Waweka dhamana wanaweza pia kuchagua kujitoa na kutoa salio lao lote la mthibitishaji. Ili kuhakikisha Ethereum ni thabiti, idadi ya wathibitishaji wanaoondoka kwa wakati mmoja imewekewa ukomo.

Takriban 0.33% ya jumla ya idadi ya wathibitishaji wanaweza kujitoa kwa siku fulani. Kwa chaguo-msingi, wathibitishaji wanne (4) wanaweza kujitoa kwa kila kipindi (kila dakika 6.4, au 900 kwa siku). Mthibitishaji mmoja (1) wa ziada anaruhusiwa kujitoa kwa kila wathibitishaji 65,536 (216) wa ziada zaidi ya 262,144 (218). Kwa mfano, kukiwa na wathibitishaji zaidi ya 327,680, watano (5) wanaweza kuondoka kwa kila kipindi (1,125 kwa siku). Sita (6) wataruhusiwa kukiwa na jumla ya idadi ya wathibitishaji wanaofanya kazi zaidi ya 393,216, na kadhalika.

Kadiri wathibitishaji wengi wanavyojitoa, idadi ya juu zaidi ya wathibitishaji wanaojitoa itapunguzwa polepole hadi kiwango cha chini cha wanne ili kuzuia kwa makusudi kiasi kikubwa kinachoweza kuvuruga uthabiti cha ETH iliyowekwa dhamana kutolewa kwa wakati mmoja.

Mchanganuo wa mfumuko wa bei baada ya unganisho

  • Jumla ya usambazaji wa ETH: ~ETH 120,520,000 (wakati wa Unganisho mnamo Septemba 2022)
  • Utoaji wa tabaka la utekelezaji: 0
  • Utoaji wa tabaka la mwafaka: Sawa na hapo juu, ~0.52% kiwango cha utoaji kwa mwaka (kukiwa na jumla ya ETH milioni 14 zilizowekwa dhamana)

Jumla ya kiwango cha utoaji kwa mwaka: ~0.52%

Upunguzaji halisi katika utoaji wa ETH wa kila mwaka: ~88.7% ((4.61% - 0.52%) / 4.61% * 100)

 Kuteketeza

Nguvu iliyo kinyume na utoaji wa ETH ni kiwango ambacho ETH inateketezwa. Ili muamala utekelezwe kwenye Ethereum, ada ya chini (inayojulikana kama "ada ya msingi") lazima ilipwe, ambayo hubadilika mfululizo (kitalu hadi kitalu) kulingana na shughuli za mtandao. Ada inalipwa kwa ETH na inahitajika ili muamala uchukuliwe kuwa halali. Ada hii inateketezwa wakati wa mchakato wa muamala, na kuiondoa kwenye mzunguko.

Kuteketeza ada kulianza kufanya kazi na sasisho la London mnamo Agosti 2021, na inabaki bila kubadilika tangu Unganisho.

Mbali na kuteketeza ada kulikotekelezwa na sasisho la London, wathibitishaji wanaweza pia kupata adhabu kwa kuwa nje ya mtandao, au mbaya zaidi, wanaweza kukatwa kwa kukiuka sheria maalum zinazotishia usalama wa mtandao. Adhabu hizi husababisha kupunguzwa kwa ETH kutoka kwenye salio la mthibitishaji huyo, ambayo haitolewi moja kwa moja kama tuzo kwa akaunti nyingine yoyote, na hivyo kuiteketeza/kuiondoa kwenye mzunguko.

Kuhesabu wastani wa bei ya gesi kwa kushuka kwa bei

Kama ilivyojadiliwa hapo juu, kiasi cha ETH kinachotolewa kwa siku fulani kinategemea jumla ya ETH iliyowekwa dhamana. Wakati wa kuandika haya, hii ni takriban ETH 1700 kwa siku.

Ili kubaini wastani wa bei ya gesi inayohitajika kufidia kikamilifu utoaji huu katika kipindi fulani cha saa 24, tutaanza kwa kuhesabu jumla ya idadi ya vitalu kwa siku, kwa kuzingatia muda wa kitalu wa sekunde 12:

  • (1 block / 12 seconds) * (60 seconds/minute) = 5 blocks/minute
  • (5 blocks/minute) * (60 minutes/hour) = 300 blocks/hour
  • (300 blocks/hour) * (24 hours/day) = 7200 blocks/day

Kila kitalu kinalenga 15x10^6 gas/block (zaidi kuhusu gesi). Kwa kutumia hii, tunaweza kutatua wastani wa bei ya gesi (katika vipimo vya Gwei/gesi) inayohitajika kufidia utoaji, kwa kuzingatia jumla ya utoaji wa ETH wa kila siku wa ETH 1700:

  • 7200 blocks/day * 15x10^6 gas/block * Y gwei/gas * 1 ETH/ 10^9 gwei = 1700 ETH/day

Kutatua kwa Y:

  • Y = (1700(10^9))/(7200 * 15(10^6)) = (17x10^3)/(72 * 15) = 16 gwei (kuzungusha kwa tarakimu mbili tu muhimu)

Njia nyingine ya kupanga upya hatua hii ya mwisho itakuwa kubadilisha 1700 na kigezo X kinachowakilisha utoaji wa ETH wa kila siku, na kurahisisha iliyosalia kuwa:

  • Y = (X(10^3)/(7200 * 15)) = X/108

Tunaweza kurahisisha na kuandika hii kama utendakazi wa X:

  • f(X) = X/108 ambapo X ni utoaji wa ETH wa kila siku, na f(X) inawakilisha bei ya Gwei/gesi inayohitajika kufidia ETH yote mpya iliyotolewa.

Kwa hivyo, kwa mfano, ikiwa X (utoaji wa ETH wa kila siku) utapanda hadi 1800 kulingana na jumla ya ETH iliyowekwa dhamana, f(X) (Gwei inayohitajika kufidia utoaji wote) itakuwa 17 gwei (kwa kutumia tarakimu 2 muhimu)

Usomaji zaidi